Miezi saba ni mwezi mmoja tu baada ya kumwanzishia mtoto chakula. Hii ina maana kuwa unaelewa ni chakula kipi kinaweza kumpa aleji na hivyo kuepukana nacho. Hata hivyo kusoma juu ya chakula kipi unafaa kuongeza ama kubadilisha ni safari ambayo haina mwisho. Tunaangazia chakula cha mtoto wa miezi saba.
Mambo Ya Kuzingatia Kuhusu Ya Chakula Cha Mtoto Wa Miezi Saba

Endelea kunyonyesha na pia mpatie chakula chenye madini ya chuma. Mtoto alishwe kwa ratiba inayoeleweka kila siku. Katika hiyo ratiba hakikisha angalau mara moja kwa siku muda wake wa kula unakuwa sawa na muda wa familia yote ili muweze kula pamoja.
Vyakula vyake viwe vimepondwa pondwa kabisa ikiwezekana kwa kutumia blender. Hakikisha anapata mlo kamili yani matunda, mboga mboga, mbegu, nafaka, nyama na samaki. Inashauriwa kutochanganya aina tofauti za nafaka kwenye unga mmoja unapotengeneza uji.
Pika aina moja ya uji kwa wakati, unaweza kufanya kwa wiki au unavyopenda.Unapompa mboga na matunda anza na tunda moja kwa wakati. Matunda kama papai,parachichi na embe ni mazuri kwa kuanzia. Chemsha maharagwe, njegere au mboga za majani na kumpa supu kidogo kidogo.
Usiweke chumvi nyingi kidogo sana inatosha. Usimpe mtoto sharubati zilizotengenezwa. Hakikisha unamtengenezea juisi wewe mwenyewe. Usichanganye matunda mbalimbali kwenye juisi moja na usiweke sukari kabisa.
Jinsi Ya Kutengeneza Chakula Cha Mtoto Wa Miezi Saba

Ni rahisi sana kutengeneza chakula cha mtoto nyumbani kwako. Osha mikono yako vizuri kabla ya kuandaa chakula na hakikisha unatumia vyombo safi.
Osha mboga zako vizuri kwa maji safi ya vugu vugu. Kisha katakata na kubandika jikoni kwa chumvi kidogo sana bila mafuta. Ikichemka isage kwenye blender au ponda ponda iwe laini kabisa kisha mpe mtoto. Matunda osha pia kwa maji ya uvugu vugu, toa ganda la nje na kata vipande vikubwa kama unataka ale kwa mikono yake mwenyewe au ponda ponda kisha mpe kwa kijiko.
Chemsha vipande vya nyama kwa maji kidogo. Iive kwa moto wa kiasi hadi ilainike kabisa. Uisage kwenye mashine kisha umpe na ile supu. Samaki vile vile ila samaki hakuna haja ya kuisaga maana ikiva inalainika sana na ni rahisi kwa mtoto bila taabu.
Hapa nazungumzia maharagwe, kunde, njegere. Pika hadi ziive kabisa na kulainika kisha pondaponda na kumpa mtoto. Pia viazi na ndizi vinafaa sana kwa watoto, unaweza ukachanganya na supu ya samaki au maziwa.
Usalama Katika Chakula
- Hakikisha haumuachi mtoto mdogo na chakula au kinywaji bila uangalizi hata kama ni maziwa ya chupa asije akapaliwa
- Usimpe mtoto chakula au maziwa akiwa amelala, analia ama anacheka
- Usimpe chakula ambacho kinaweza kumkaba au kumpalia kama karanga, mahindi
- Kabla ya kumpa mtoto chakula hakikisha umekiangalia joto lake usije ukamuunguza mdomo
- Usafi wa mtayarishaji, mlishaji na mlishwaji ni muhimu sana
Chakula cha mtoto wa miezi saba ni kigumu kuliko hapo awali. Pia ni kingi kuliko unapomwanzishia. Sababu kuu kwa nini mtoto huanzishiwa chakula kwa utaratibu ni kuwa mfumo wake wa kusaga chakula bado unazoea.
Chanzo: WebMD
Soma Pia:Mlishe Mtoto Wako Vyakula Hivi Ili Kuhimiza Kurefuka Kwake!