Hapo awali, watu walipata watoto walipokuwa wangali wachanga. Ila, siku hizi, mambo yamechukua mkondo tofauti. Watu wanachukua muda zaidi kabla ya kuanzisha familia na kuwa wazazi. Kuna mambo mengi ambayo yamechangia katika mabadiliko haya. Kama vile ukuaji wa teknolojia mpya. Teknolojia za kisasa zinawawezesha watu kupata habari kuhusu mambo yanayo fanyika pande tofauti za dunia. Mojawapo ya mambo haya yakiwa kufahamu matatizo ambayo wazazi hupitia. Kifedha na kihisia hasa kama hawakuwa tayari kuwa wazazi. Tofauti na hapo awali ambapo wazazi hawakuwa huru sana na watoto wao kuhusu familia na uzalishaji, siku hizi ujumbe huu wote upo mitandaoni. Watu wanachukua muda kujitayarisha vyema zaidi kabla ya kuanza mkondo huu mpya maishani. Tazama dalili za kuwa tayari kuwa mzazi.
Dalili Za Kuwa Tayari Kuwa Mzazi

- Maisha yako yana uimara
Watoto wanahitaji mazingira imara. Ikiwa ungali unahisi kuwa unasumbuka kulipa baadhi ya gharama zako za kimaisha, huenda ikawa sio wakati sawa kwako kupata mtoto.
Watoto ni gharama kubwa. Wana mahitaji mengi, ya kimavazi, kijitanda, kulipia kliniki, neppi na zinginezo. Hata kama unahisi kuwa kihisia umejitayarisha vilivyo kuwa mzazi, iwapo fedha zako bado zinasumbua, sio wakati mwema kwako kupata mtoto. Chukua muda huu kuhifadhi na kuwekeza fedha zako ili utakapo pata mtoto, uwe na uwezo wa kukimu mahitaji yake.
2. Unaweza kujitunza
Huwezi sema kuwa uko tayari kuwa mzazi ilhali bado unatatizika kufanya mambo yako. Kama kupanga vitu utakavyovifanya kwa siku. Unapokuwa mzazi, utahitajika kufanya mambo mengi kwa pamoja. Chukua kila fursa unayopata mtoto anapolala kufanya kazi zako.
Ikiwa unawatarajia watu wengine kukufanyia vitu vyako ama kukusaidia kutosheleza mahitaji yako ya kifedha, bila shaka hauko tayari kuwa mzazi.
3. Hauogopi majukumu

Kadri unavyozidi kuzeeka, ndivyo unavyopata majukumu zaidi. Majukumu ambayo haukuwa tayari kugharamia. Sote huwa na wakati ambapo tunahisi hatutaki kwenda kazini, tunataka kupumzika siku hiyo. Hata hivyo, kuwa mtu mzima kuna maana kuwa unawajibika kuenda kazini hata siku unapohisi uzembe.
Unapokuwa mzazi, unapata majukumu mengi. Kulea watoto hakuna likizo, ni kazi inayo endelea hata wanapokuwa watu wazima na kuishi makwao. Unapohisi kuwa uko tayari kufanya kazi ya ulezi kila siku hata usipokuwa na hisia za kufanya hivyo, uko tayari kuwa mzazi.
4. Umefanya uamuzi wa kupata mtoto
Kupata mtoto kunapaswa kuwa kwa hiari yako, sio kufuatia kulazimishwa na mchumba wako, familia ama shinikizo la wanarika wako. Ama hata kwa ajali bila kupangia safari hii kubwa.
Kulingana na jamii, kupata mtoto ni jambo la kawaida. Ni vyema kuelewa kuwa sio kila mtu anaye azimia kuwa mzazi, na ni sawa. Na kwa wale wanaotamani kuwa wazazi, uamuzi huu unapaswa kuwa wa kibinafsi bila kusukumwa kufanya hivi. Hakikisha kuwa unaangazia vidokezo tulivyotaja kabla ya kufanya uamuzi wa kuwa mzazi. Tunakutakia mema katika safari ya kuwa mzazi!
Soma Pia: Kuboresha Uhusiano Kati Ya Mzazi Na Mtoto: Vidokezo Muhimu Kutoka Kwa Zozibini Tunzi