Mzazi anapomtishia mtoto, mara nyingi mtoto hujitenga na mzazi, na kuleta kutofautiana kati ya mzazi na mtoto. Kuna mbinu tofauti za kuboresha uhusiano kati ya mzazi na mtoto ambazo wazazi wanaweza kutumia. Hasa wanapogundua kuwa mtoto anajitenga na hazungumzi nao baada ya kukosolewa.
Kuboresha uhusiano kati ya mzazi na mtoto

Kuwa na maelewano
Ili kuepuka athari hasi za kumtishia mtoto wako, mnaweza kuwa na maelewano. Kwa mfano, iwapo mtoto wako hajafanya kazi ulizompatia, badala ya kumtishia, mweleze kuwa hataweza kutazama runinga hadi anapofanya kazi zile. Ama, anihitajika kuwa nyumbani kwa saa fulani ama wakati unapomhitaji kukamilisha kazi zile. Mweleze mtoto wako umuhimu wa kufuata maagizo, elewa kwa nini hakuweza kumaliza kazi zile kisha muwe na maelewano.
Mhimize
Kwa kawaida, watoto hutaka kuwafurahisha wazazi wao. Wanataka kuhisi kuwa wana uhusiano wa karibu na wazazi wao, kuwa wamekubalika na wanapendwa. Wanataka kuhisi kuwa wana uwezo wa kufanya chochote wanachotaka maishani. Tumia hii kwa njia inayofaa. Badala ya kumtishia mtoto anapokosea, elewa kuwa huenda hakujua kuwa anachofanya ni kibaya. Fikiria kuhusu utakacho mwambia. Usitumie lugha yenye makali.
Zungumza kwa ukarimu

Jinsi unavyomzungumzia mtoto ni muhimu zaidi kuliko maneno unayomwambia. Epuka kutumia maneno makali, zungumza kwa upole unapomweleza alipokosea. Zungumza kwa njia inayomhimiza na kumrekebisha na kuhisi kuwa hata kama alikosea, bado anapendwa na yeye ni muhimu kwako. Mkumbatie hata anapokosea na unapomrekebisha.
Mfunze
Ikiwa ungependa mtoto wako asirudie kosa alilofanya, njia ya kipekee ni kumfunza jinsi ya kufanya jambo hilo. Kwa mfano, ikiwa amevunja sahani akiosha, mwonyeshe jinsi ya kushika sahani, ama umpe sahani zisizoweza kuvunjika.
Kuwa na wakati tosha wa familia
Kuwa na wakati tosha na familia kila siku kunadumisha uhusiano wako na watoto. Kwa njia hii, hata unapomrekebisha mtoto, anahisi kuwa anarekebishwa na rafiki yake. Kuwa na dakika 30 kila siku za kucheza na kuzungumza na watoto wako kuna himiza uhusiano wenu.
Kukuza ujasiri wa mtoto wako
Wapatie watoto wako majukumu ambapo wanaweza kufuzu na kujenga ujasiri wao. Majukumu na kuchangia katika kazi za nyumbani ni njia nzuri ya kukuza ujasiri wa mtoto. Wanahisi kuwa wanakubalika, kuthaminiwa na ni sehemu kuu ya familia yao.
Punguza wasaa wa kutazama televisheni
Kutazama runinga wakati wote kwa watoto huanzisha matatizo mengi. Watoto wanapokuwa wachanga, kuzoea kuwa kwenye televisheni wakati wote ama simu huibua matatizo kama kuwa na ujeuri. Unapomkataza, huenda akakataa kukusikiliza. Kumpa majukumu anapotazama televisheni pia kutaibua vurugu, kwani anataka kuendelea kutazama runinga.
Chanzo: WebMD
Soma Pia: Matatizo Mbalimbali Yanayo Kumbuka Ulezi