Jinsi ya kujua kuwa una mimba kwa kufanya kipimo cha mimba kunafahamika zaidi. Ila, mwanamke anaweza kuangazia dalili za mapema za mimba kufahamu iwapo ana ujauzito ama la. Kumbuka kuwa mwanamke anaweza kuwa na ishara za mapema za ujauzito na kukosa mjamzito. Baadhi ya dalili za ujauzito kama kuumwa na tumbo na kuhisi uchovu mara kwa mara zinafanana na dalili za hedhi kukaribia.
Jinsi Ya Kujua Una Mimba: Kuangazia Dalili Za Mimba
- Kukosa kipindi cha hedhi

Mzunguko wa hedhi wa kila mwezi huwa njia ya mwili kujitayarisha kubeba mimba. Kuta ya uterasi inakuwa nene ili yai lililorutubishwa lipate mahali pa kujipandiza. Mwanamke asipopata mimba, kuta hii huporomoka na kutolewa mwilini kama hedhi. Iwapo mwanamke ana mimba, kuta hii inabaki na mwanamke kukosa kipindi cha hedhi. Mwanamke anaweza kosa kupata hedhi anaposafiri, kubadilisha mazingira yake, kubadilisha lishe, kufanya mazoezi magumu ama kuwa na mawazo mengi.
2. Kuvuja damu nyepesi
Damu ya implantation huonekana wakati sawa na mwanamke anapotarajia kipindi chake cha hedhi. Damu hii ni ishara kuwa yai lililorutubishwa limejipandikiza kwenye uterasi ya mama. Mama asipokuwa na ufahamu, huenda akadhani hii ni damu ya hedhi. Damu ya hedhi na ya implantation huwa na tofauti. Wakati ambapo damu ya hedhi huwa nyingi na yenye rangi nyekundu iliyokolea, damu ya implantation huwa nyepesi, haijazi pedi na yenye rangi ya pinki.
3. Maumivu upande wa chini wa tumbo

Maumivu ya aina hii huenda yakawa ishara kuwa hedhi inakaribia. Huenda yakaashiria yai kujipandikiza kwenye uterasi. Kwa baadhi ya wanawake, maumivu haya huambatana na kuvuja damu ya implantation, wakati ambapo wanawake wengine kamwe hawapati damu ya implantation. Maumivu haya huja na kuisha baada ya muda kwa siku chache.
4. Mabadiliko kwenye maziwa
Katika ujauzito, maziwa ya mama hubadilika kufuatia ongezeko la vichocheo mwilini. Vichocheo vya estrogen na progesterone huchangia katika maziwa kuwa laini zaidi na kufura.
5. Uchovu
Uchovu mwingi ni ishara inayoshuhudiwa katika muhula wa kwanza wa ujauzito. Kwa kiwango cha wanawake, hii huwa dalili inayowafahamisha kuwa wana mimba. Ongezeko la kichocheo cha progesterone humfanya mama kuhisi amechoka saa zote. Ni vyema kwa mjamzito kulala na kupata mapumziko tosha.
Chanzo: Healthline
Soma Pia: Vidokezo 5 Vya Kuwa Na Ujauzito Salama Na Wenye Afya