Uhusiano wenye afya kati ya mzazi na mtoto unafanyika mzazi anaposhuka kwenye hadhi ya kuongoza na kuwalinda watoto na kuanza kuwaona kama watu wanaotoshana kihadhi, alisema mtaalum Carder Stout. Mipaka yenye afya na wazazi ni muhimu. Ili kufika katika hatua hii, wazazi wanapaswa kuelewa kuwa watoto wao wamekua na wana uwezo wa kufanya uamuzi dhabiti maishani mwao. Watoto pia wanapaswa kuelewa kuwa wazazi wao ni binadamu na wana doa zao.
Haijalishi umri wako, kuna baadhi ya wazazi ambao watajaribu kufanya uamuzi maishani mwako. Kukwambia unachostahili kufanya maishani hata bila kuomba ushauri wao. Kukushauri unachopaswa kufanya katika uhusiano wako na mchumba wako ama watoto.
Wazazi kuhusika zaidi na maisha yako huwa kufuatia mapenzi kwako. Huenda wakahisi kuwa uhuru wako unakutenga nao na wangependa kubaki maishani mwako. Na kuhisi kuwa wanafahamu zaidi unachohitaji maishani mwako, hili sio kweli. Wazazi wanapohusika maishani mwako kwa njia usizofurahia, wanapiku mipaka na kuweka uhusiano wenu kwenye laini kwa njia hasi.
Vidokezo hivi vinasaidia kusisitiza mipaka yenye afya na wazazi wako

- Zungumza nao
Njia ya kipekee ya kufahamu kinachoendelea na wazazi wako ni kwa kuzungumza nao. Kumbuka kuwa jinsi unavyozungumza na sauti unayoitumia ni muhimu. Waulize kuhusu hofu zao, ikiwa wanakupigia mara kwa mara hata unapokuwa kazini, nafasi kubwa ni kuwa wanahisi upweke. Waeleze kuwa unakua, una mambo mengi ya kufanya lakini hata maisha yako yanapobadilika, wahakikishie kuwa hawako peke yao. Kuwa na masuala hasa ambayo ungependa kuzungumzia nao unapoanza mazungumzo haya.
2. Sisitiza mipaka yako kwa upendo na heshima
Wazazi huenda wakasahau kuwa mtoto wao sio mtoto tena na ana uwezo wa kuishi maisha yake bila usaidizi wao. Washukuru kwa kukulea, na kukuonyesha njia maishani. Kisha uwaeleze mipaka yako kwa heshima na kuwa itakuwa ishara ya heshima wanapoangazia unachowaambia. Waeleze kuwa walitia juhudi kukulea na ni wakati wa kuamini kuwa walifanya kazi bora na kuwacha uishi maisha yako sasa.
3. Kuwa mahususi kuhusu shaka zako
Katika tamaduni za kiafrika, kuna imani kuwa wazazi huwa sawa wakati wote. Ni makosa kubishana na wazazi ama kuwaeleza wanapokosea. Usihisi hatia unapozungumza kuhusu mipaka yako. Huenda likawa halitakuwa jambo rahisi, lakini litasaidia kudumisha uhusiano kati ya mzazi na mwanawe. Kuwa na masuala mahususi ambayo ungependa wazazi wako warekebishe kisha uyazungumzie bila hofu.

4. Kumbuka umuhimu wa mipaka
Kukosa mipaka husababisha mambo hasi kama chuki kati ya wazazi na watoto, kukasirika ovyo ama hofu ya kuzungumza. Hata kama kuwaeleza wazazi mipaka yako huenda kukawafanya wakasirike ama wahisi hawapendwi, baada ya muda, wataheshimu mipaka yako na kuiangazia. Kukosa kuzungumza wazazi wanapofanya mambo yasiyokufarahisha, kutafanya ukose kuzungumza nao ama kutowatembelea.
5. Fahamu wakati wa kujitenga
Baada ya kuzungumza na wazazi na kuona kuwa hawaheshimu mipaka yako. Unaweza kujitenga na wao kwa muda. Kutoheshimu mipaka ya watu huenda kukaathiri afya yao ya kiakili. Unaweza kuwaambia kitu kama, "ungefurahia wasipokutembelea kwa muda fulani kwani unataka wakati wako wa kipekee."
Kuwa na mipaka yenye afya kunasaidia kudumisha uhusiano wenye afya kati ya wazazi na watoto. Kutosheleza mahitaji yako ya kipekee ya kihisia, kifizikia na kiakili na hata kuboresha uhusiano wenu. Mipaka inakulinda kwa hivyo ni muhimu kuwa na mipaka mahususi wakati wote na watu wote.
Soma Pia: Hali Ya Gharama Ya Maisha Nchini Kenya Na Vyanzo Vyake