Uzazi huwa jambo ngumu, hasa kwa sababu hakuna kanuni bora za ulezi hasa zinazopaswa kufuatwa. Hakuna anayejua ulezi unaofaa, ila kila mzazi hufanya juhudi kadri awezavyo kuhakikisha kuwa anawalea watoto wake kwa njia bora zaidi. Tazama kanuni hizi za kijumla ambazo kila mzazi anaweza kufuata.
Kanuni za ulezi bora

- Unachofanya ni muhimu
Watoto huiga tabia za wavyele wao, na wala sio maneno yao. Ni muhimu kwa mzazi kuhakikisha kuwa vitendo vyake vinaendana na maneno yake. Unachokifanya, unavyokuwa miongoni mwa watu wengi, kuwa mtu mwenye nidhamu na heshima kwa watu wengine. Bila shaka watoto watakua wakiwaheshimu watu wengine. Usiseme unachotarajia wafanye, mbali anza kwa kuwa mfano wa kuigwa.
2. Wapende watoto wako
Hakuna kiwango cha mapenzi ambacho mzazi hapaswi kupita inapofika kwa kuwapenda watoto wake. Hilo ndilo jukumu kubwa zaidi alilonalo, kuhakikisha kuwa watoto wanahisi mapenzi ya mzazi wake. Kumpenda mtoto hakumaanishi kumnunulia vitu vyote anavyovitaka. La hasha, kumbuka kuwa wazazi wana uwezo tofauti wa kifedha.
3. Husika maishani mwa mtoto wako
Kuwa mzazi 'active' maishani mwa mtoto wako huwa na athari chanya maishani mwake na hata anapokomaa. Kuhusika maishani mwa mtoto huchukua juhudi na wakati kumpa mtoto kipaumbele. Badala ya kwenda kutembea na marafiki, unachukua wasaa huo kuwa na watoto wako. Kufika nyumbani mapema baada ya kazi na kuwasaidia watoto wako kufanya kazi za ziada, kucheza, kula pamoja nao na hata kuhusika na masomo yao.

4. Mlee mtoto wako kulingana na mahitaji yake
Kosa kubwa ambalo wazazi wengi hufanya ni kuwalea watoto wao kutumia mwongozo wa wazazi wao. Ama kwa njia sawa na walivyolewa na wazazi wao. Ukweli ni kuwa, kila mtoto huwa na mahitaji tofauti na mwingine. Ni vyema kwa mzazi kuelewa mahitaji ya kila mtoto, kisha kumpa ulezi unaomfaa.
5. Kuwa na masharti
Kuna usemi maarufu kuwa, 'mtoto umleavyo ndivyo akuavyo'. Masharti unayomfunza mtoto akiwa mdogo ndiyo atakayofuata anapokua. Ikiwa kuna baadhi ya vitu usivyovipendelea anavyovifanya akiwa mchanga, mrekebishe. Samaki mkunje angali mchanga, ili akue akijua anachopaswa kufanya na asichostahili kufanya.
6. Endeleza uhuru wake
Kumhimiza mtoto kuwa huru hukuza kujiamini na kumsaidia kuwa na imani kuwa anaweza kutegemea uamuzi wake kufanya mambo yoyote yale maishani. Badala ya kumkazia mtoto, mpe uhuru ili anapokuwa na suala, aje kuomba usaidizi wako.
7. Kuwa rafiki yake
Mbali na kuwa mzazi wa mwanao, ni muhimu kwa wazazi kuwa na urafiki na watoto wao. Kwa njia hii, anaposumbuliwa na jambo, atakuja kuzungumza nawe kusikia maoni yako. Watoto wanapoogopa wazazi wao, huendea ushauri kwa marafiki zao, ushauri unaopotosha.
Soma pia: Athari Za Uchovu Wa Ulezi Kwa Wachumba Na Watoto