Mapenzi matamu yanapokuwa ya kweli. Ila, yanapokuwa bandia yanaleta maumivu mengi ya moyo. Baada ya kuwachwa ama kutendwa na mchumba, huenda ikawa vigumu kuwaamini watu. Hasa wanapotaka kuanzia mahusiano ya kimapenzi. Kuna hofu kuwa huenda wakakutenda kama wapenzi wa hapo awali. Kuweza kubaini kati ya mapenzi bandia na ya kweli kutakulinda dhidi ya kuumizwa moyo.
Je, utawezaje kubaini iwapo mtu anakupenda ama anacheza na hisia zako kisha kutokomea baada ya kupata anachotaka kutoka kwako?
Ili kuweza kufahamu ikiwa mtu ana nia nzuri, kuwa makini kuangalia ishara hizi.
Ishara za Mapenzi Bandia

- Kukuwacha ufanye kila kitu
Uhusiano huwa ushirikiano kati ya watu wawili. Wakati unapohisi kuwa umewachiliwa kufanya mambo yote peke yako. Kufanya uamuzi muhimu bila usaidizi wala mwingine kujali iwapo ungetaka kusaidiwa ama la. Kutwikwa majukumu yote kama vile kupanga wakati wa kupatana, mahali pa kupatana, masaa na kuwa wewe ndiye unayetoa pendekezo la kupatana wakati wote. Hakuna mapenzi ya kweli. Mtu anayekupenda atakusaidia unapotaka usaidizi na kamwe hatakuwacha kufanya mambo yote peke yako.
2. Kutokujali
Je, umekula, umeshindaje, kazi imekuwaje leo? Lipi linalo kukwaza sasa hivi? Baadhi ya maswali maarufu kati ya wapenzi. Ikiwa mtu anadai kukupenda ila matendo yake ni tofauti. Hajali unachofanya, unavyoendelea na iwapo uko salama, bila shaka hakuna mapenzi ya kweli.

3. Kutofunguka kihisia
Mtu anayekupenda atakuwa wazi kwako, kihisia. Kukueleza alivyo, anavyohisi bila kuficha lolote wala kuwa na hofu kuwa huenda ukamwumiza. Unapogundua kuwa anayesema anakupenda anakuficha vitu vingi. Hakuelezi bayana anavyohisi kuhusu vitu tofauti, ukweli ni kuwa hana mapenzi kwako. Mazungumzo kati ya watu wanaopendana kwa kwa kweli huwa wazi bila kuficha chochote.
4. Hatii juhudi kukuona
Mtu anayekupenda atatia juhudi kukuona mara kwa mara. Unapogundua kuwa hatii juhudi zozote kupatana nawe, fahamu kuwa hayo ni mapenzi bandia. Mtu anayekutaka atatia juhudi kukuona kwani ni dakika hizi zinazoboresha utangamano wenu.
5. Maneno na matendo kuwa tofauti
Unapogundua kuwa maneno na matendo ya mtu hayana uiano, hiyo ni ishara ya onyo. Nafasi kubwa ni kuwa maneno yake ni bure tu. Hakupendi jinsi anavyosema kuwa anakupenda. Kuwa makini kuhakikisha kuwa anafanya anachosema kuwa atatenda.
Soma Pia: Ishara 5 Kuwa Msichana Anakupenda Kwa Sababu ya Pesa Ila Sio Mapenzi