Makala haya yanazungumzia vidokezo muhimu vya kumsaidia mwanamke aliye katika umri wake wa kupata watoto. Ikiwa unahisi kwamba huu ni wakati bora wa kuanza familia, vidokezo hivi vitakusaidia kuboresha uwezo wa kushika mimba chini ya miezi miwili.
Vidokezo vya kuboresha uwezo wa uzalishaji

- Wasiliana na mtaalum wa afya ya kike
Asilimia 40 ya wanawake huwa na nafasi ya kutunga mimba chini ya miezi miwili wanapofanya ngono bila kinga. Kabla ya kuanza juhudi za kushika mimba, ni vyema wakati wowote ule mwanamke kuwasiliana na mtaalum wa afya ya kike. Hasa miezi mitatu hadi sita kabla ya wakati anapopanga kutunga mimba. Vipimo kabla ya kutunga mimba vinamsaidia mwanamke kujua hali yake ya afya na iwapo kuna mabadiliko anayostahili kufanya kabla ya kushika mimba.
Baadhi ya vipimo vinavyofanyika ni kama vile:
Kipimo cha ujumla. Kudhibitisha iwapo wazazi wote wana matatizo yoyote ya kiafya.
Kipimo cha afya ya uzazi. Kipimo cha pap ama pelviki kinafanyika kubaini afya ya uzazi ya mwanamke.
Vipimo vya maambukizi ya kingono. Kutibiwa maambukizi haya kuna boresha nafasi za mwanamke za kutunga mimba.
2. Zingatia afya bora
Kwa wanandoa ambao wangependa kutunga mimba, ni muhimu kuwa makini na afya yao na kuhakikisha kuwa wanazingatia mitindo bora ya kiafya. La kwanza ni kupunguza utumiaji wa vileo na ikiwezekana kuvitupilia mbali. Kisha kujitenga na utumiaji wa sigara. Zina uwezo wa kupunguza nafasi za kutunga mimba kwa kuathiri afya ya mfumo wa uzazi na mishipa ya damu.
3. Kula lishe bora
Ili kuutayarisha mwili kubeba mtoto, mwanamke anastahili kuutunza zaidi na mojawapo ya njia za kufanya hivi ni kwa kula lishe bora. Kuhakikisha kuwa mwili unapata virutubisho tosha. Mbali na mwili wa mama kupata nguvu za kuusaidia kubeba mimba, mtoto atapata virutubisho tosha kumsaidia kukua ipasavyo.
Kupunguza ulaji wa vyakula vilivyo kaangwa kwa mafuta nyingi, vyakula vilivyo na sukari nyingi. Kupunguza ulaji wa wanga nyingi na ngano nyingi pia ni muhimu.
4. Kufanya mazoezi

Kufanya mazoezi mara kwa mara kunausaidia mwili kustahili safari ya mimba na kujifungua. Mama anashauriwa kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki kwa dakika 30-45. Ikiwezekana, kufanya mazoezi kila siku ya wiki ni bora. Mwili unapata nguvu zaidi za kustahimili mabadiliko yanayofanyika katika mimba.
5. Fahamu siku zako za kupevuka kwa yai
Ikiwa ungependa kutunga mimba kwa kasi, fahamu mzunguko wa hedhi na siku ya kupevuka kwa yai. Mara nyingi, hii huwa siku ya kumi na nne baada ya kuanza kwa kipindi chako cha hedhi. Wanandoa wanapofanya mapenzi bila kinga katika siku hii, wana nafasi zaidi za kutunga mimba. Wasiliana na daktari wako ikiwa una tatizika kufahamu siku ya kupevuka kwa yai.
Ni muhimu kwa wanandoa kukumbuka kuwa maisha huwa hayaendi kulingana na mipango yao. Na mara nyingi mambo hufanyika tofauti na tunavyo tarajia. Kuwa wavumilivu na msikate tamaa katika juhudi zenu za kutafuta mtoto na mzidi kutumia mbinu hizi za kuboresha uwezo wa kushika mimba.
Chanzo: WebMD
Soma Pia: Kuharibika Kwa Mimba Na Umuhimu Wa Kusafisha Mji Wa Uzazi