Imedhihirika kuwa ni vigumu kulewa watoto bila wao kukukasirisha katika wakati mmoja ama mwingine, ama asilimia 50 ya wakati. Mzazi ni binadamu kama watu wengine. Wana matatizo ya kimaisha, kazi kando na majukumu ya kinyumbani na gharama za kulipa. Kwa hivyo katikati ya nyakati hizi, mtoto wako anaweza kufanya kosa na kufuatia fikira zote mzazi alizonazo, ahisi hasira nyingi. Tazama baadhi ya vidokezo vya kudhibiti hasira yako kama mzazi.
Jinsi Ya Kudhibiti Hasira Yako Kama Mzazi

- Tulia kwanza kabla ya hatua
Hasira ni hisia inayowasukuma binadamu kutaka kuchukua hatua kwa kasi. Kwa hivyo, ili kuepuka kuchukua hatua bila kufanya uamuzi wa kina, chukua muda utulie kwanza. Inasaidia kufahamu jinsi ambavyo hasira hufanya kazi na kujikumbusha kupumua ama hata kutabasamu. Kutabasamu ama kuumua kunasaidia kubadili hali ya hisia zako. Kutabasamu hutuma ujumbe kwa ubongo wako kuwa hali sio ya dharura. Kisha mwili wako unaanza kutulia.
Kwa baadhi ya watu, huenda wakahitaji njia ya kutoa hasira zao. Kama kubadili mazingira na kwenda chumbani kingine. Ikiwa wewe ni baadhi ya watu ambao lazima wagonge kitu ili kujituliza, jaribu kugonga mto. Usifanye hivi mbele ya watoto wako.
2. Chukua dakika moja
Unapojipata umekasirishwa na tabia za wanao ukiwa nyumbani, chukua dakika moja uende nje. Hasira huziba fikira za mtu, kwa hivyo chochote ufanyacho dakika hiyo, huenda ukajuta baadaye. Kwa wazazi wengi, hasa wa Afrika, kuna imani kuwa ukimwomba mtoto wako radhi, kuna maana kuwa wewe ni mnyonge na ameshinda. Sio kweli. Kuondoka kunamzungumzia mtoto wako undani wa kosa lake na kuwa unaweza kujidhibiti.
3. Ahirisha kumpa nidhamu
Kumpa mtoto nidhamu sio lazima kuwa dakika moja baada ya kufanya kosa. Hatapotea, na bila shaka hata anapokimbia na kwenda kwa shangazi yake, atarudi kwako jioni. Zungumza naye na umweleze kuwa hujapendelea alichofanya, kisha umweleze kuwa utafikiria kuhusu adhabu utakayo mpa.

4. Chochote kinachofanyika, usimgonge mtoto wako
Ni vigumu kupata mzazi wa kiafrika ambaye hajawahi kumgonga mtoto wake baada ya kukasirishwa. Hili ni la kizazi kijacho, kwa wanaopanga kupata watoto.
Nguvu za kifizikia sio njia bora ya kumpa mtoto wako nidhamu. Huenda ukahisi vyema baada ya kumgonga mtoto na kutoa hasira zako. Badala yake, tumia vidokezo tulivyoangazia hapo awali. Kadri unavyotoa hasira yako kwa kumgonga mtoto wako, ndivyo unavyozidi kuzoea kufanya hizi.
5. Epuka kutumia vitisho
Ni rahisi kufuata mkondo wa kumtishia mtoto wako kila anapokosea na kukukasirisha. Maneno makali kama vile, "nitakuchapa uzirahi, nitakuua leo, utanifahamu leo". Haya ni maneno ambayo wazazi wengi hutumia watoto wanapokosea, ila sio vyema. Kumbuka kuwa maneno unayoyatumia ndiyo watoto wako watakayo yatumia wanapoenda nje ya nyumba yako. Sio sawa.
Hitimisho
Ikiwa baada ya kujaribu haya yote ungali una hasira, inasaidia kukumbuka kuwa, hasira ni njia ya kujikinga ambayo binadamu hutumia kujilinda dhidi ya hisia kama vile hofu ama uwoga. Tafuta chanzo cha hasira. Una hofu ya nini? Nini unachokiogopa? Kufahamu haya kutakusaidia kutulia na kuchukua mkondo tofauti kumpa mtoto wako nidhamu. Hisia hizi zikizidi, mtafute mshauri.
Tengeneza orodha ya njia zinazokubalika za kukabiliana na hasira. Zungumza na watoto wako pia. Wafahamishe kinachokubalika na kisichokubalika. Mnaweza kutengeneza orodha hii kwa pamoja.
Soma Pia: Vidokezo Vya Kuwa Mzazi Bora