Kukomesha Umbeya Kwa Watoto Wadogo

Kukomesha Umbeya Kwa Watoto Wadogo

Kuna mambo mengi sana yanayo tendeka mtoto anapokuwa shuleni. Mojawapo ya mambo haya ni uvumi na umbeya ambao unasambaa kwa sana miongoni mwa watoto. Kuna mengi unayo weza kumlinda mtoto wako dhidi ya, ila mengine huwezi. Ila, unaweza kumfunza jinsi ya kukabaliana na mambo tofauti ili kumwepusha kuwa muadhiriwa. Kama vile umbeya ambao huwezi mlinda mtoto wako kutokana nao ila unaweza mfunza jinsi ya kukabiliana na hali hii. Cha kuhuzunisha kuhusu umbeya ni kuwa, wakati mmoja watakuwa wanaongea kuhusu yaliyo tendeka, wakati mwingine mwanafunzi mwingine na dakika inayo fuata, watakuwa wana mwongelelea mtoto wako. Kwa sababu ya haya, unapaswa kumtayarisha mtoto wako kukabiliana na mambo haya.

Kukomesha Umbeya Kwa Watoto Wadogo

Picha: Shutterstock

Kukabiliana na Umbeya kwa watoto

Jua Kisa na maana cha umbeya ule

Mtoto wako anapokwambia kuwa watoto wengine walimsengenya shuleni, jambo la kwanza ni kumwuliza chanzo cha umbeya huo. Walikuwa kwa mada gani kabla ya kuanza kumwongelelea vibaya. Aliye anza uvumi huo alikuwa na dhamira gani? Je, aliwasingizia wengine kumfuata na kuongea vibaya kuhusu mtoto wako? Ni muhimu kwa mtoto wako kujua haya kabla ya kukabiliana na jambo hili.

Mfunze mtoto wako kusema ‘hapana’

Marafiki wake shuleni wanapokuja kumpatia uvumi mfunze kusema ‘hapana’ bila woga. Kwa njia hii, watoto wengine wataheshimu msimamo wake dhidi ya umbeya. Asipo waunga mkono kwa kusikiza uvumi kuhusu watoto wengine, uwezekano ni kuwa watoto hawa pia wata aibika kusambaza umbeya kwa watoto wengine kumhusu. Pia unaweza mhimiza kuuliza yeyote anaye mpatia umbeya ‘mbona unaniambia haya’. Kwa njia hii, anaye mpatia umbeya ataaibika kumpatia habari nyingi kuhusu watu wengine.

Mhimize mtoto wako asikae sana kwa umbeya

Kwa mara nyingi, jambo hili huwa rahisi zaidi kusema kuliko kutenda. Ni muhimu sana kwa mtoto wako kuto weka umuhimu zaidi kwa uvumi. Ili kufanya hivi, mhimize awe na marafiki wasio unga mkono umbeya shuleni. Pia, anapaswa kuwa kioo cha jambo hili kwa kuto wasengenya wengine. Anapokuwa shuleni, jambo la muhimu kuzingatia ni masomo na michezo. Kisa na maana, uvumi hasi huwa na athari hasi kwenye ukuaji wa mtoto wako. Huenda akajitenga ama kufeli kwenye mitihani yake ama hata kuchukia masomo. Hakikisha pia unapo kuwa nyumbani, unamhusisha kwa kazi za kinyumbani ambapo atakuwa na jambo la kufanya wakati wote na hana muda wa kufikiria mabaya.

kupunguza umbeya kwa watoto

Epuka kuto mshauri unapokuwa na hasira

Ni kawaida kwa kila mzazi kukasirika anaposikia kuwa watoto wengine wana sambaza umbeya kwa watoto wengine kumhusu. Huenda wakati huu kwa kuwa na hasira nyingi ukamshauri mtoto wako kufanya mambo ambayo si mema sana kwani unafuata hasira zako. Jambo la kwanza ni kuhakikisha kuwa unajituliza kabla ya kumshauri mwanao. Kwa sababu mtoto wako atafuata matendo yako zaidi ya atakavyo fuata utakacho mwambia. Chukua muda wako na utulie. Kisha, mhusishe mtoto wako kwenye mjadala na uweze kujua mbona watoto wengine shuleni walikuwa wana sambaza uvumi kumhusu. Kuwa na mjadala mpana naye hadi ujue chanzo cha mambo hayo yote. Mwulize anavyo hisi kuhusu jambo hilo. Kwa wakati huu, hasira zako zitakuwa zimepungua, mshauri kama mama na umhimize kuto weka marafiki ambao kazi yao siku yote kazi yao ni kusambaza uvumi.

Mfunze mtoto wako athari za kusambaza umbeya

Mtoto anapo elewa athari za kusambaza umbeya kutoka kwa umri mchanga, anaepuka kuwa chanzo cha hisia mbaya kwa watu wengine. Sisitiza kuwa umbeya hufanya watoto wengine wahisi vibaya ama kuwafanya kujitenga na jamii ambalo ni jambo hasi. Mwulize jinsi angehisi ikiwa yeye ndiye aliyekuwa akiongelelewa vibaya na watu wengine. Ikiwa hangefurahi, aelewe kuwa mtoto mwenzake hatafurahi akifanyiwa jambo hilo. Kwa hivyo ajitenge tabia hiyo hasi. Sisitiza kuwa kutumia wakati wake shuleni akisambaza uvumi kuhusu watu wengine ni kupoteza muda na kutamfanya afeli kwenye vitabu na maishani.

umbeya kwa watoto

Picha: Shutterstock

Mfunze kusimama kama mshumaa

Wakati ambapo kila mtu anafuata mkondo, mfunze mwanao kusimama kidete na kukataa kuwa miongoni mwa watu wanao sambaza uvumi kuhusu watoto na watu wengine. Asimame ang’ae kama mshumaa na awaonyeshe wengine njia iliyo sawa kufuata.

Mfunze kunyamaza

Sio lazima aongee wengine wanapo ongea na kuwa kunyamaza ni dhahabu. Akisikia wengine wanasambaza uvumi ama wanaongea vibaya kumhusu, mhimize anyamaze na awaonyeshe kisogo chake. Badala ya kujihusisha kwenye mambo mabaya, ni vyema kunyamaza. Mkumbushe kuwa mtu akimpatia uvumi kuhusu watu wengine, ataenda kusambaza umbeya kumhusu kwa watu wengine.

Unaweza mfunza mtoto wako mengi ila usipo fuata unacho mwambia, hatayatilia maanani maneno yako. Kwa hivyo mama, unataka mtoto wako kukaa mbali na umbeya na wambeya? Je, wewe mwenyewe ni mbeya? Ongoza kwa mfano, ikiwa hapo awali umekuwa na tabia ya kuongea kuhusu marafiki wako na mtoto wako ako karibu, KOMA! Koma hiyo tabia kwa sababu, kadri unavyo zidi kusambaza uvumi kuhusu watu wengine na mtoto wako yuko, hatawacha tabia hii. Kwa hivyo, kuwa mfano wa kuigwa mzazi! Fuata mambo unayo mwambia mtoto wako kuyafanya. Je, ungependa awache kusambaza uvumi shuleni? Koma basi kusambaza uvumi kuhusu wengine.

Na bila shaka mtoto wako atakusikiza na kuishi maisha ya kuigwa na wenzake pale shuleni kwani anaufuata mfano wako na sio maneno tu mbali na matendo yako pia!

Vyanzo: QDT, kidshealth

Written by

Risper Nyakio