Kila mtoto anapolia, unampakata na baadhi ya wakati huenda ukawa unamshika zaidi kuliko unavyomlaza. Mara nyingi mzazi mpya anapofanya hivi, atasikia mamake mzazi ama mtu mwingine aliye na watoto wakubwa akimkemea. Na kumwambia kuwa kufanya hivyo kunamdekeza mtoto. Usimshike mtoto sana, unamharibu, mzazi mpya atasikia akiambiwa mara nyingi. Je, ni kweli kuwa kumshika mtoto sana kunamharibu?
Kumshika mtoto kunamdekeza?

Hii ni imani isiyo ya kweli inayozidi kupitishwa kwa vizazi. Hata baada ya utafiti unaoegemezwa na wataalum kuwa huwezi kumharibu mtoto mchanga, wazazi bado wanazidi kushikilia imani kuwa kumpakata mtoto sana kunamdekeza. Masomo yaliyofanyika katika nyanja hii yamedhihirisha kuwa kumshika mtoto kwa muda mrefu kunapunguza mara anazolia.
Hakuna uwezekano wa kumharibu mtoto mchanga kwani akili yake ingali inakua na haelewi kinacho endelea.
Mzazi anapaswa kumwacha mtoto alie bila kumshika?
Wazazi wa hapo awali waliamini kuwa mtoto hapaswi kupakatwa mara tu anapolia. Anastahili kuwachiliwa alie kwa muda. Kulingana na utafiti, watoto waliowachwa kulia kwa muda kabla ya kupakatwa hawakuwa na matatizo ya kulia kwa sana walipotengana na wazazi wao katika umri wa mwaka mmoja. Hata hivyo, ni vigumu kwa wazazi hasa wa mara ya kwanza kuwaacha watoto wao walie kwa kipindi kirefu.
Kushughulikia mahitaji ya mtoto mchanga sio kumharibu

Ni vyema kushughulikia mahitaji ya mtoto anapotaka na katika umri huo mchanga, sio kumharibu, mbali ni kumpa anachohitaji. Mama anapoelewa kila kilio cha mtoto na maana yake anaweza kufahamu mtoto anachotaka. Kuna kilio cha uchovu, cha njaa na cha kubadilishwa nepi.
Mtoto anapofikisha miezi sita kisha kuendelea kudekezwa, ana nafasi za juu za kuharibika. Katika umri huu, ni vyema kwa mama kufahamu mahitaji ya kimsingi na yasiyo ya kimsingi na kupunguza kumpatia vitu ambavyo sio vya kimsingi. Ili kupunguza nafasi za kumdekeza na kumharibu.
Mtoto angali mchanga, mama hapaswi kuwa na wasiwasi kuwa kumshika mtoto sana kunamharibu hasa kila mara anapolia ama kumnyonyesha mara kwa mara. Kumshika na kuwa na mguso wa ngozi kunasaidia kuboresha utangamano kati ya mzazi na mwanawe.
Chanzo: WebMd
Soma Pia: Kuwatenganisha Watoto: Faida Na Hasara Za Kujifungua Mtoto Wa Pili Baada Ya Miaka Fulani