Ni furaha ya kila mama kupatana na mwanawe. Hata ingawa mchakato wa kujifungua huwa mrefu na mgumu, anapompakata mwanawe kwa mara ya kwanza, furaha anayohisi hupanguza machozi ya safari hiyo. Baada ya kubeba mtoto kwa miezi tisa, mwili huchoka, kujifungua kupitia kwa upasuaji wa c-section humfanya mama kukosa nguvu zaidi. Kidonda cha c-section huchukua muda zaidi kupona ikilinganishwa na kujifungua kwa njia ya kawaida. Tuna angazia baadhi ya mbinu za jinsi ya kupona kwa kasi baada ya c-section.
Tazama vidokezo ambavyo vitamsaidia mama kupona kwa kasi baada ya c-section

Upasuaji wa c-section ni sawa na aina yoyote ile ya upasuaji mkubwa. Mwili wa mama unahitaji muda ili upone. Mara nyingi, mama hubaki hospitalini kwa siku tatu ama nne baada ya kumpata mwanawe ili mwili upumzike. Baada ya hapo, mwili utachukua angalau wiki sita ama zaidi kupona.
Mama huwa na uchungu mwingi anapotembea, kupanda ngazi, kuchemua ama kucheka. Anashauriwa baada ya upasuaji huu kupumzika na kupata usaidizi kufanya kazi nyumbani. Pia ni vyema kwake kutofanya kazi zinazompasa kuinama ama kubeba vitu vizito. Mbali na hayo, mama anapaswa kupata masaa tosha ya usingizi kwa siku.
Katika kipindi hiki, mama anapaswa kuutunza mwili wake zaidi hadi apone. Mama huwa na majukumu mengi. Hata anapokuwa mgonjwa, mara nyingi, atajipata akihitajika kufanya baadhi ya kazi za nyumbani. Hasa anapojifungua, kazi kama kumbadili mtoto nepi na kupika chakula chake. Ikiwezekana, mama anaweza pata msaidizi katika kipindi hiki hadi atakapopona.
Jitenge kufanya mazoezi hadi mwili wako upone. Chukua chakula laini ambacho hakitakufanya uvimbiwe ama utatizike kwenda msalani.

- Kuwa mwangalifu wa lishe yako
Safari ya kula lishe bora haiishi unapojifungua, la hasha, sawa na ulivyozingatia lishe bora katika ujauzito, ni muhimu kwa mama kuwa makini na lishe hata baada ya kujifungua. Kumbuka kuwa mtoto anategemea lishe ya mama ili apate virutubisho bora mwilini. Hakikisha sahani yako wakati wote ina mboga za kijani, matunda kisha unywe maji tosha.
- Kunywa dawa za kutuliza uchungu
Mama anapotoka hospitalini, mara nyingi atapatiwa dawa za kupunguza uchungu. Kunyonyesha mtoto baada ya upasuaji wa c-section huwa na uchungu. Dawa hizi husaidia kupunguza kiwango cha uchungu.
Chanzo: WebMD
Soma Pia: Jinsi Ya Kuhakikisha Kuwa Kidonda Chako Cha C-section Kinapona Mbio