Je, wanawake wajawazito wanaweza kunywa kahawa na vinywaji vyenye kaffeini? Wataalum huwashauri wanawake wajawazito kupunguza unywaji wa kaffeini. Ikiwezekana wachukue chini ya miligramu 200 za kaffeini kwa siku. Ni muhimu kupunguza unywaji wa kaffeini katika mimba, utafiti unaonyesha kuwa hata viwango vidogo vya kaffeini huenda vikaathiri mtoto. Kumbuka kuwa kaffeini haipatikani kwa kahawa tu, mbali kuna vyakula vingine vilivyo na kaffeini, kwa hivyo ni vyema kusoma label za vyakula. Je, madhara ya kaffeini katika mimba ni yapi?
Madhara Ya Kaffeini Katika Mimba

Mwanamke mjamzito anaweza kunywa kahawa?
Naam, mwanamke mjamzito anaweza kunywa kahawa. Walakini, anastahili kupunguza kiwango cha kahawa na bidhaa za kaffeini anazochukua anapokuwa na mimba.
Kiwango cha kaffeini kilicho salama katika mimba
Mama mjamzito anashauriwa kunywa miligramu 200 za kaffeini kwa siku ama chini yake. Hata hivyo kuna shaka kuwa viwango vya chini huanzisha hatari kwa mtoto anayekua tumboni. Unywaji mwingi wa kaffeini umehusishwa na tatizo la Intrauterine Growth Restriction (IUGR) katika watoto. Kulingana na utafiti, wanawake wanaochukua hata viwango vya chini vya kaffeini wanajifungua watoto wadogo ikilinganishwa na wanawake wasiokunywa kahawa katika mimba.
Unywaji wa kaffeini katika mimba umehusishwa na kubana kwa placenta na mishipa ya damu kwenye uterasi. Na kupunguza kiwango cha damu kinachofika kwenye fetusi na kusababisha ukuaji wa fetusi kukwama.
Kaffeini katika mimba inahusishwa na kuathiri homoni za ukuaji wa fetusi, jambo linalosababisha watoto kuongeza uzani kwa kasi baada ya kujifungua.
Ongezeko la uzito kwa kasi linawaweka watoto katika hatari ya kuugua maradhi ya moyo na kisukari baadaye maishani.
Athari za Kaffeini katika ujauzito kwa mama

- Mwanamke mjamzito anapokunywa kaffeini, inapita kwenye placenta hadi kwa amniotic fluid na kisha kwenye mfumo wa damu wa mtoto
- Kwa mama, kaffeini itaongeza mpigo wake wa moyo na shinikizo la damu
- Kumkosesha usingizi usiku
- Kuongeza hali ya kiungulia
- Mama kupata haja ya kwenda msalani mara kwa mara
Vyakula vilivyo na kaffeini vya kuepuka katika mimba
Kahawa, chai, soda, chokleti, vinywaji vya kuongeza nishati kama red bull.
Sio rahisi kwa mama kutupilia mbali unywaji wa kaffeini hasa kama alikuwa amezoea kabla ya kushika mimba. Anaweza kujaribu mambo haya:
- Kupunguza kiwango cha kaffeini anachokichukua kwa siku. Baada ya muda ataweza kuacha kutumia kaffeini na bidhaa zake
- Kujaribu kuchanganya vinywaji visivyo na kaffeini nyingi. Kama vile kupika kahawa na kisha kuongeza maziwa. Kutumia kiwango kidogo cha kahawa
- Kuchukua vinywaji mbadala kama vile chai ya kijani badala ya kahawa na vinywaji vya kaffeini
Mama anapokuwa na shaka kuhusu vyakula vyovyote vile, ni vyema kuwasiliana na daktari wake ampe ushauri.
Chanzo: WebMD
Soma Pia: Umuhimu Wa Lishe Bora Mapema Katika Mimba Ni Upi?