Mazungumzo kuhusu fedha sio baadhi ya mazungumzo yenye starehe zaidi. Hasa na mtu unayependa, huenda ukawa na shaka nyingi na kujiuliza iwapo yataadhiri uhusiano wenu. Hata hivyo, ni muhimu kuzungumzia fedha kabla ya kuingia katika ndoa. Tazama baadhi ya mazungumzo muhimu kuhusu fedha unayopaswa kuangazia na mwenzio kabla ya kufunga ndoa.
Mazungumzo Muhimu Kuhusu Fedha Unayopaswa Kuangazia na Mwenzio Kabla ya Kufunga Ndoa

- Je, tuna utangamano wa kifedha
Ndoa huja baada ya kuwa katika uchumba na mpenzi wako kwa muda. Katika kipindi hiki, unaweza kuangalia tabia zake za kifedha na kufahamu uhusiano alio nao na pesa. Huenda kuna vitu anavyofanya na pesa zake na hata baada ya kuangalia mienendo yake, lazima uulize maswali ili kujua zaidi. Swali la utangamano wa kifedha linakusaidia kujua mambo anayoyapatia kipau mbele na iwapo yanaendana na unayoyathamini pesa zinapohusika.
Je, mchumba wako anaamini kuhifadhi kiwango fulani cha pesa kwanza kabla ya kutumia pesa zinazobaki ama anatumia pesa kisha kuhifadhi zinazobaki?
2. Je, una deni?
Baadhi ya watu wengi waliosomea vyuo vikuu nchini Kenya wana madeni ya wanafunzi. Hizi ni fedha ambazo kila mwanafunzi aliyefuzu na kwenda katika chuo kikuu hupatiwa kumsaidia kulipa karo ya shule na kupata kiwango kidogo cha pesa za mfukoni. Baada ya kuhitimu, kila mwanafunzi anatarajiwa kuanza kulipa deni lake. Kufahamu deni za mpenzi wako kabla ya kufunga ndoa kutawawezesha kupanga fedha zenu kwa njia inayowawezesha kukamilisha deni hizi kwanza.
Je, deni zake ni kufuatia deni la wanafunzi, ununuzi wa mali ama kununua vitu vinavyopunguka dhamani.
3. Majukumu ya kifedha
Je, kuna wanafamilia wanaokutegemea kulipa bili zao kila mwezi. Huenda ikawa ni karo ya ndugu, wazazi kutarajia kutumiwa pesa za matumizi ama kulipiwa kodi na kadhalika. Kufahamu majukumu ya kifedha ya mpenzi wako yatawasaidia kujua mtakavyo panga fedha zenu na iwapo baadhi ya majukumu hayo ni muhimu ama yanaweza kupunguzwa.

4. Kugawanya bili za nyumba
Mazungumzo muhimu kabla ya kufunga ndoa. Yanakuwezesha kujua iwapo mna malengo tofauti. Kuingia katika ndoa na majukumu dhabiti kunasaidia kuepuka matatizo ya siku za usoni kuhusu fedha. Kufahamu mchumba atakaye lipa kodi, karo ya shule, vyakula na kadhalika kunasaidia kuhakikisha mna utangamano wa kifedha.
5. Je, tutakuwa na akaunti moja ya fedha ama tofauti
Kuwa na uhusiano wa ndani kuna maanisha kuwa na mazungumzo magumu hasa ya kifedha. Je, mtakuwa mnahifadhi pesa zenu kwenye akaunti moja ama kila mtu atakuwa naye. Kufahamu jambo hili kutawasaidia kufahamu mtakavyojipanga mnapokuwa na fikira za kuwekeza katika sekta fulani.
Soma Pia: Ushauri Wa Kindoa Ulio Muhimu Kwa Wanandoa Wote