Mwanamke mwenye mimba ama anayefikiria kupata mimba anafahamu mambo ya kimsingi anayopaswa kujua kuhusu mimba. Kama kutovuta sigara ama kunywa pombe. Licha ya kutofanya kazi ngumu, tunaangazia vidokezo vya mimba salama na yenye afya.
Vidokezo vya Mimba Salama na Yenye Afya
1. Chukua vitamini za prenatal

Vitamini za prenatal ni muhimu katika kuhakikisha kuwa fetusi inakua kwa njia ipasavyo. Kuilinda dhidi ya kupata matatizo ya neural tube, ya kiakili ama uti wa mgongo. Mjamzito anapaswa kuanza kuchukua vitamini za prenatal miezi michache kabla ya kupata mimba, ama punde tu anapofahamu kuwa ana mimba. Vitamini za prenatal zina virutubisho muhimu kama kalisi, chuma na asidi ya folic.
2. Jifunze kuhusu ujauzito na kuwa mama
Kila ujauzito huwa wa kipekee. Haijalishi iwapo wewe ni mama wa mara ya pili ama ya tano, kuchukua darasa kuhusu kujifungua na kuwa mama ni muhimu. Kunakutayarisha kwa mchakato wa kujifungua na kuondoa hofu inayoandamana na mchakato huu. Kuwa na mkunga wa kujibu maswali ya kiujauzito kunakusaidia kufahamu jambo jipya kila mara.
3. Badilisha majukumu ya kikazi
Baadhi ya majukumu huwa hatari katika mimba. Kusafisha uchafu wa paka kunamweka mama mjamzito katika hatari ya kupata maradhi. Kazi zinazohusisha kugusa kemikali zinahatarisha maisha ya fetusi. Ikiwa kazi inahusisha kusimama kwa muda mrefu, huu ni wakati bora wa kubadilisha majukumu ya kikazi.
4. Fanya mazoezi

Kufanya mazoezi kuna manufaa mengi kwa mjamzito. Kuboresha mzunguko wa damu mwilini, kupunguza mawazo mengi, kupunguza uchungu mwilini, kusaidia kulala vyema zaidi usiku na kuboresha hisia za mama. Mama mjamzito anapaswa kufanya kazi kwa karibu na mtaalum wa mazoezi hasa kama mimba yake ni ya hatari. Kufanya mazoezi mepesi kwa dakika 30-45 kuna manufaa mengi kwa mama na mtoto.
5. Kuwa makini na vitu vyenye sumu
Vileo, pombe, sigara, dawa za kulevya huwa vyanzo vya matatizo ya kiafya katika mimba. Sigara hupunguza kiwango cha hewa kinachomfikia mtoto na kusababisha kujifungua kabla ya muda. Vileo vimehusishwa na kujifungua mtoto aliye na uzani wa chini ama matatizo ya kuchelewa katika ukuaji wake.
6. Kunya maji
Mjamzito anahitajika kunywa maji zaidi katika kipindi hiki. Ili kuwezesha utendakazi mwilini wa kuzungusha virutubisho na hewa mwilini na kwa mtoto na kutoa uchafu kutoka kwa mtoto kwa mama na kuupitisha nje ya mwili. Maji yanakinga dhidi ya kuvimbiwa, kufura miguu ama maumivu ya mara kwa mara.
7. Kula samaki

Samaki ni chanzo bora cha omega-3, iliyo muhimu katika ukuaji wa ubongo. Kula samaki katika mimba kunasaidia na ukuaji wa ubongo wa mtoto. Hata hivyo, kuna aina ya samaki wenye zebaki nyingi, kama vile swordfish na mackerel. Kwa sababu hii, mama anashauriwa kuwasiliana na mtaalum wa afya kufahamu samaki bora. Wanaoshauriwa ni tuna, shrimps na salmon.
Ili kuhakikisha kuwa mama ana mimba salama na yenye afya, ni muhimu kuzingatia mitindo bora ya maisha. Lishe bora, kujitenga na unywaji wa vileo na kutofanya majukumu yanayohusisha kugusa kemikali.
Chanzo: WebMD
Soma Pia: Aina 3 za Anemia Katika Mimba na Jinsi ya Kuziepuka