Huu ndiyo mwezi bora zaidi katika safari yako ya mimba. Kwa sasa tumbo inaonekana vizuri, mtoto ameanza kurusha mateke tumboni, na uso wako una ng'ara. Kuna mengi ya kutarajia katika mimba ya miezi 5, tazama!
Mimba ya Miezi 5

Kulingana na uzito na misuli yako, huenda tumbo yako ikawa kubwa katika mwezi huu ama bado ndogo. Usiwe na hofu! Hakuna uzito hasa ambao wanawake wote katika miezi mitano ya ujauzito wanapaswa kuwa wakipima. Uzito wako katika mwezi huu unaathiriwa pakubwa na uzito uliokuwa nao kabla ya kutunga mimba. Kupoteza uzito kwa kasi katika mimba ni ishara hasi na unapaswa kuzungumza na daktari wako kuhakikisha kuwa kila kitu kiko shwari.
Ishara za mimba katika mwezi wa 5
Katika mwezi huu, hamu yako ya kula huwa nyingi na kuchangia pakubwa katika ongezeko lako la uzito wa mwili. Utashuhudia kuwa uso wako una ng'ara na kucha na nywele zako kumea kwa kasi kuliko ilivyo kawaida. Ishara katika mwezi huu ni kama vile:
- Maumivu ya mgongo
- Kuhisi kizunguzungu
- Chuchu kukolea rangi na kuwa nyeusi zaidi
- Kiungulia
- Kuumwa na miguu
- Kuvimba miguu
- Mapua kushikana ama kuwa na homa
- Kuvimbiwa
Ukuaji wa fetusi katika mwezi wa tano

Katika mwezi huu, mtoto wako ana uzito wa ounsi 10 na urefu wa inchi kati ya 6 na 7. Ngozi yake kwa sasa imekuwa na inaweza kumlinda. Nywele kinywani zimeanza kumea katika mwezi huu na huenda akawa ameanza kunyonya kidole cha gumba.
Mwendo wa fetusi katika miezi mitano
Kwa sasa, utaanza kuhisi mtoto wako akirusha mateke tumboni. Ikiwa bado hujaanza ni sawa, baada ya muda mfupi utaanza kuhisi mwanao akirusha mateke. Katika wiki 28 za ujauzito, unaweza kuanza kuhesabu mateke mwanao anayoyarusha.
Kudumisha afya katika mwezi wa tano wa mimba
Mazoezi ni muhimu katika mimba. Yanakusaidia kuwa na afya bora, kukuepusha dhidi ya kuongeza uzito wa kupindukia, kukusaidia kulala vizuri usiku na kupunguza uvimbe kwenye miguu. Kwa hivyo, hakikisha kuwa unafanya mazoezi mara kwa mara hata kama ni kutembea kwa dakika 30 kwa siku.
Ikiwa ulikuwa unafanya mazoezi magumu kabla ya kupata mimba, punguza kiwango cha mazoezi unayoyafanya katika kipindi hiki na hasa katika miezi ya kwanza ya mimba. Ikiwa unaanza kufanya mazoezi katika mimba, anza kwa mazoezi mepesi kwa kipindi kifupi. Ni vyema kufanya mazoezi haya kwa usaidizi wa mtaalum. Kuna baadhi ya mazoezi hatari kwa mama mjamzito. Mazoezi salama katika mimba ni kama vile:
- Kutembea
- Kuogelea
- Darasa za densi
- Kunyoosha mwili
- Yoga
Zingatia lishe yenye afya katika kipindi hiki ili mtoto apate virutubisho muhimu vya kudumisha ukuaji wake.
Chanzo: WebMD
Soma Pia: Jinsi Ya Kuboresha Lishe Na Siha Kwa Mama Mjamzito