Nifanye nini ili nipate usingizi? Swali maarufu kwa watu wanaotatizika na kukosa usingizi. Kukosa usingizi ni jambo linalotia shaka, hata ingawaje, sio kila mtu anayetatizika na hali hii. Kuna baadhi ya watu ambao hulala punde tu wanapoingia kitandani na kufumba macho. Huku wengine wakibaki kuimba nyimbo za kujilaza.
Kutopata usingizi huwa na athari hasi siku ifuatayo. Kama vile kupunguka kwa utendaji kazi wako, kukosa uwezo wa kumakinika na kuzingatia, kulala kazini ama darasani na kuhisi uchovu siku yote. Kabla ya kuchukua tembe za kusaidia kulala kuna njia za kiasili zinazosaidia kulala vyema usiku.
Nifanye nini ili nipate usingizi

Fanya haya ili upate usingizi:
- Tengeneza ratiba ya kulala
Kutokuwa na wakati haswa wa kuingia kitandani huwa chanzo cha kukosa usingizi. Ili kukabiliana na tatizo la kutopata usingizi usiku, ni muhimu kutengeneza ratiba ya kulala. Baini wakati ambao utakuwa ukiingia kitandani kila siku na uuzingatie kwa umakini. Kufanya hivi kutazoesha akili yako kulala wakati fulani unapofika.
2. Fanya mazoezi mchana ama jioni
Kufanya mazoezi kuna manufaa mengi kwa mwili. Mojawapo ya manufaa haya ni kusaidia kulala vyema zaidi usiku. Wakati unapofanya mazoezi, mwili huchoka na unapokoga, inakuwa rahisi kulala ili kuupumzisha mwili. Hata hivyo, kumbuka kutofanya mazoezi magumu jioni, kwani huenda yakawa na athari tofauti na tunazokusudia kutimiza.
3. Usitumie rununu kitandani

Kutumia simu kitandani kuna ashiria ubongo uendelee kufanya kazi katika wakati unapostahili kuwa ukilala. Watu wanaotumia simu usiku hasa wakiwa kitandani huenda wakatatizika kupata usingizi. Hakikisha hautumii simu ama vifaa vingine vya kiteknolojia kitandani.
4. Usilale mchana
Epuka kulala mchana, hasa kulala zaidi ya masaa mawili. Watu wanaokuwa na mazoea ya kulala kwa zaidi ya masaa mawili kwa siku wameshuhudiwa kutatizika kupata usingizi usiku. Hata unapokosa usingizi usiku, haushauriwi kulala kwa kipindi kirefu mchana. Badala yake, tafuta vitu vya kufanya ili usitatizike kulala tena usiku.
5. Epuka kutumia kaffeini na bidhaa zake usiku
Kaffeini hutumika kuamsha ubongo na kukufanya uwe makini zaidi, unapokunywa kaffeini ama bidhaa zake usiku, una athiri muundo wako wa usingizi. Punguza kiwango cha kaffeini unachochukua mchana. Ikiwa unatatizika kupata usingizi, jitenge na utumiaji wa kaffeini na bidhaa zake kwa muda.
6. Zingatia ratiba ya lishe yenye afya
Watu wanaokula chakula kingi kisha kuenda kulala muda mfupi baada yake, huenda wakatatizika kupata usingizi. Mwili huchukua muda kuchakata chakula, unapolala tu baada ya kumaliza kula, mwili ungali unakifanyia chakula kazi na huenda ukahisi kutapika ama kichefuchefu. Upe mwili wakati tosha kuchakata chakula kabla ya kulala.
7. Sikiliza muziki wa kulala
Kuna baadhi ya muziki unaosaidia kukupumzisha. Kusikiliza aina hii ya muziki unapoenda kulala, huenda kukasaidia kupata usingizi kwa kasi zaidi. Hata hivyo, ni vyema kukumbuka kuwa, siyo kila mtu anayefaidika na jambo hili.
Tuna tumai kuwa swali lako la, nifanye nini ili nipate usingizi limejibiwa. Ikiwa baada ya kutumia mbinu tulizoangazia bado unatatizika kupata usingizi, wasiliana na daktari. Huenda ukawa na matatizo ya kiafya yanayokukosesha usingizi.
Je, kuna mbinu zaidi unazofahamu za kusaidia kupata usingizi usiku? Tujulishe kwa kuwacha ujumbe mfupi hapa chini!
Chanzo: Healthline
Soma Pia: Manufaa Ya Kula Kitunguu Saumu Kwa Afya Yako