Utunzaji kwa mama baada ya kujifungua unapaswa kukabiliana na mahitaji maalum ya mwanamke. Pindi anapojifungua na kuendelea kuwepo kwa wiki sita zifuatazo. Hizi huduma ni pamoja na uzuiaji, kugundua mapema na kutibu matatizo. Huu utaratibu hufanyika ili kuhakikisha kwamba mama anapata nafuu baada ya kuzaa kimwili na kihisia.
Utunzaji Baada Ya Kujifungua

Huduma za utunzaji baada ya kujifungua hasa zinajumuisha hatua za kuzuia. Hizi hulenga kutambua mapema visababishi vya kawaida vya maradhi kwa kina mama na vifo katika Jamii. Pia utoaji wa ushauri kuhusu unyonyeshaji, upangaji uzazi, chanjo na lishe bora baada ya kujifungua. Hizi ni pamoja na:
- Chunguza ishara muhimu kwa mama
Hizi ishara ni joto lake, kiwango cha mpigo kwa mshipa na shinikizo la damu. Hii ni kuhakikisha kuwa ziko katika kiwango cha kawaida. Mara tu baada ya kujifungua, chunguza mipigo ya mama kwa mshipa na shinikizo la damu.
Ikiwa shinikizo la damu yake iko chini mno na inashuka na mipigo yake inapiga kwa haraka anaelekea kuwa na mshtuko. Kama hakuna dalili ya kutokwa na damu ukeni, anaweza kuwa anapoteza damu ndani ya mwili wake.
- Chunguza kama uterasi yake ina mikazo ya kawaida
Gusa fumbatio lake kupima mikazo ya uterasi ili kuhakikisha kwamba iko imara. Mara tu baada ya kujifungua unapaswa kuwa na uwezo wa kuhisi mikazo karibu na kitovu cha mama. Na kuteremka chini katika pelvisi yake kwa mwendo wa kasi zaidi kwa wiki mbili zijazo.
Chunguza uterasi yake kila baada ya dakika 15 kwa masaa mawili baada ya kujifungua. Iwapo uterasi ni ngumu iwache wakati wa vipimo. Ikiwa utahisi ikiwa laini sugua fumbatio juu ya uterasi ili kusaidia iwe na mikazo.
Image: Kiera Nelson/Facebook
- Safisha tumbo ya mama, viungo vya uzazi na miguu
Msaidie mama kujisafisha baada ya kujifungua. Badilisha matandiko yoyote yale chafu na usafishe damu iliyo mwilini mwake. Nawa mikono kwanza na uvae glavu kila mara kabla ya kugusa viungo vya uzazi wa mama ili kumlinda kutokana na maambukizi.
Safisha viungo vyake kwa utaratibu kwa kutumia sabuni na maji safi na kitambaa safi. Usitumie kemikali ya kuua viini vya maradhi yoyote ambayo inaweza kuwasha tishu nyororo.
- Chunguza uvujaji wa damu nyingi
Baada ya kujifungua, ni kawaida mama kutokwa na damu kiasi sawa na ya hedhi. Mara ya kwanza damu hutoka au kumwagika wakati uterasi inakaza ama mama anapokohoa. Baada ya siku mbili, mtiririko unafaa kupungua. Kutokwa na damu nyingi ni ishara ya hatari.
- Chunguza viungo vya uzazi vya mama iwapo kuna miraruko na matatizo mengine
Tumia mkono ulio na glavu kwa utaratibu kuchunguza viungo vya uzazi vya mama kwa miraruko, vibonge vya damu au hematoma. Ikiwa mwanamke ana mraruko unaohitaji kushonwa hakikisha kuwa mama amepata hio huduma.
Kuna mraruko mwingine ni mdogo hauhitaji kushonwa. Elekeza juu ya utunzaji bora kuhakikisha nafuu ya haraka. Chunguza kama seviksi imechomoza. Tatizo hili si hatari na kwa kawaida hurudi ndani baada ya siku chache. Elekeza mama kufanya mazoezi ya kukaza misuli ya uke na kuta za pelvisi angalau kwa mara nne kwa siku.
Kujaliwa mtoto ni jambo ambalo huathiri maumbile ya mama kwa hali kubwa. Hivyo utunzaji kwa mama baada ya kujifungua sio tu pendekezo lakini jambo la msingi.
Soma Pia: Wakati Bora Wa Kupata Mimba Punde Tu Baada Ya Kujifungua