Kulala kwa masaa machache na kufanya kazi kwa masaa zaidi kunasifika na kuonekana kama jambo la kutiliwa maanani. Wanaofanya hivi wanaonekana shupavu na watu wa kuigwa katika jamii. Ila katika masomo ya kliniki, hili ni jambo hasi linalopaswa kukemewa. Kutopata usingizi tosha wa masaa manane kwa siku ni hatari kwa afya na mwili. Kabla ya kuchukua tembe za kuratibisha mfumo wako wa usingizi, kuna mengi unayoweza kufanya nyumbani, kama ulaji wa vyakula vya kuleta usingizi.
Athari hasi za kutopata usingizi tosha

Kutolala vyema usiku na kuupa mwili wakati tosha wa kupona baada ya siku nzima ya kufanya kazi na shughuli tofauti huwa na athari hasi. Mwili huathiriwa kwa njia zifuatazo:
- Kuathiri ongezeko kubwa la uzani wa mwili
- Kusababisha kisukari
- Kulegea kazini
- Kukosa umakini masomoni na kazini
Vyakula vya kuleta usingizi
- Maziwa yenye joto

Kunywa maziwa yenye joto muda kabla ya kulala kumedhihirishwa kuwa na athari chanya katika kusaidia kupata usingizi. Maziwa huwa na misombo inayoboresha kupata usingizi, kama vile: kalisi, tryptophan, melatonin na vitamini D. Kunywa maziwa kabla ya kulala husaidia kupumzisha mwili na kulala vyema zaidi.
2. Almonds

Almonds zimedhihirishwa kuwa na kiwango kikubwa cha kichocheo cha melatonin kinachosaidia kudhibiti mfumo wa kulala. Almonds zina kalisi na magnesiumu zinazosaidia kuboresha kulala vyema zaidi usiku. Almonds zina afya kwani zina wingi wa ufuta mzuri na kiwango cha chini cha sukari.
3. Chai ya chamomile

Hapo zamani, mmea wa chamomile ulitumika kuponya kutopata usingizi usiku. Msimbo wa apigenin unaopatikana kwenye mmea huu unasaidia kuleta usingizi. Kunywa kikombe kimoja cha chai ya chamomile kabla ya kulala kunasaidia kulala vyema zaidi.
4. Samaki

Samaki ni chanzo kizuri cha vitamini D na pia ina omega-3 fatty acids zote ambazo zinasaidia kuboresha usingizi. Msimbo wa serotonin unaopatikana kwenye samaki unasaidia kutengeneza mfumo bora wa kulala na kuamka. Kula samaki kama vile salmon kwa wiki moja kuna athari chanya kwenye mfumo wa kulala.
5. Viazi vitamu

Viazi vitamu vya kuoka vina potassium, kalisi na magnesiamu. Zote ambazo zinasaidia kupumzika. Kula kipande cha kiazi kitamu kabla ya kulala kunasaidia kupumzisha mwili na kuwezesha kulala vyema usiku.
Mbali na kula vyakula hivi, ni vyema kufanya haya:
- Kufanya mazoezi mara kwa mara
- Kujitenga na ulaji wa chakula chenye sukari nyingi muda mfupi kabla ya kulala
- Kuepuka ulaji wa chakula kingi hasa chenye wanga dakika chache kabla ya kulala
- Kunywa maji tosha kwa siku, glasi nane ni bora
- Kujipa masaa mawili ama matatu kabla ya kulala baada ya kula chajio
- Kuepuka unywaji wa vileo kabla ya kulala
Soma Pia: Usingizi Wa Mtoto: Mambo Ya Kufanya Na Kuto Fanya