Kufanya kazi za kinyumbani na watoto kunawasaidia kuwajibika maishani. Pia wanafahamu kuwa ni jukumu lao kusaidia na wala sio kungoja kufanyiwa kazi zote wakati wote. Kufanya hivi kunawasaidia watoto hata wanapoanza maisha yao ya kikazi, kufanya kazi kama timu moja. Watoto kusaidia na kazi za kinyumbani kunawasaidia kuwa wanajamii bora. Tazama baadhi ya kazi za kinyumbani ambazo unaweza kuwahusisha watoto wako!
Watoto kusaidia na kazi za kinyumbani

Wapatie wanao jukumu la kutengeneza vitanda vyao jambo la kwanza baada ya kuamka. Wafunze kusafisha vyombo na nyumba, na uwahimize kupanga vidoli vyao wanapomaliza kucheza navyo.
Kwa njia hii, watoto wanakua wakifahamu kuwa wanapaswa kuwajibika na kusaidia katika kazi za kinyumbani bila kungoja kufanyiwa kazi wakati wote.

Unapotayarisha chakula, waulize watoto wako wakusaidie na kazi rahisi kama vile kuosha vyombo na mboga ama kupanga sahani mezani kabla ya kupakua chakula. Baada ya kumaliza kula, waulize wakusaidie kubeba vyombo na kuvipeleka jikoni. Kwa sababu wangali wachanga, waulize wakusaidie na vyombo visivyo weza kuvunjika na visivyo hatari kwao kama visu.
Dunia imebadilika na tofauti na hapo awali ambapo watu walifua nguo zao, siku hizi kuna mashine za kusaidia na kazi hizi. Kutumia mashine wakati wote kutawafanya watoto wakue bila kufahamu jinsi ambavyo nguo zinafuliwa. Hata kama una mashine ya kufua, ni vyema mara kwa mara kuwafunza jinsi ya kutenga nguo chafu kisha kuzisafisha. Unapofua mavazi yako, waulize wakusaidie kusafisha vitu vyepesi kama vile soksi.
Watoto wanapaswa kufahamu kazi zote, kunawasaidia kuwa watu wanaowajibika maishani. Wazazi wanapofanya kazi za shambani kama vile kulima, kupalilia mimea na kutoa magugu shambani, ni vyema kuwahusisha watoto. Usikubali wabaki nyumbani unapofanya kazi hizi. Hata kama hawatafanya kazi nyingi, wanavyozidi kukua watakuwa na furaha kusaidia katika kazi za kinyumbani bila ubaguzi.
Ni vyema kwa wazazi kuwafunza watoto wa jinsia zote mbili uwajibikaji. Kuna visa ambavyo wazazi hawakubalishi watoto wa jinsia moja kufanya baadhi ya kazi, huku jinsia nyingine ikitwikwa majukumu yote. Kwa mfano, baadhi ya familia hawaamini kuwa vijana wanapaswa kuingia jikoni. Kazi zote za jikoni zikibaki kufanywa na mabinti. Imani hii imepitwa na wakati, na sote tunataka kuishi kwa dunia ambapo wanaume hawaogopi kuingia jikoni hata wanapofunga ndoa. Imani tunazo walea watoto nazo ndizo wanazozibeba uzimani wao.
Watoto wote, wa kike kwa waume wanapaswa kusaidia na kazi za jikoni na pia shambani kwa usawa. Hivi basi, watoto hawa wanafahamu kuwa hakuna kazi iliyotengewa jinsia moja. Kunawasaidia pia kujituma maishani wanapokuwa wakubwa.
Chanzo: WebMd
Soma Pia: Jukumu La Baba Katika Familia Na Maisha Ya Watoto Wake